8 Februari 2015 - 19:40
Boko Haram yaushambulia mji wa Diffa, Niger

Kundi la Boko Haram limefanya shambulizi usiku wa kuamkia leo katika mji wa Diffa uliopo katika mpaka na Niger. Hii ni mara ya pili kwa Niger kushambuliwa na kundi hilo la magaidi kutoka Nigeria.

Kundi la Boko Haram limefanya shambulizi usiku wa kuamkia leo katika mji wa Diffa uliopo katika mpaka na Niger. Hii ni mara ya pili kwa Niger kushambuliwa na kundi hilo la magaidi kutoka Nigeria. Shambulizi hilo lilianza Jumamosi usiku na mapigano kati ya Boko Haram na jeshi la Niger yaliendelea hadi saa kumi na moja alfajiri ya leo, kabla wapiganaji hao kulazimika kukimbia na utulivu kurejea mjini humo. Duru za kijeshi zimesema leo kwamba mapigano makali yaliendelea karibu na daraja la kuingilia Nigeria. Mkaazi mmoja amesema bomu lililipuka katika soko la katikati mwa mji wa Diffa, lakini watu wengi walikuwa wameondoka kuyakimbia mapigano. Mtu mmoja ameuwawa na wengine 10 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.

Wakati huo huo serikali ya Marekani imelaani hatua ya kuuahirisha uchaguzi wa rais na bunge nchini Nigeria, ikidai pana ujiingizaji wa kisiasa katika kazi za tume ya uchaguzi. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema Marekani imevunjwa moyo na uamuzi wa kuahirisha uchaguzi wa rais kutoka Februari 14 hadi Machi 28. Katika taarifa yake Kerry amesema ni muhimu kwa serikali kutotumia wasiwasi uliopo kuhusu usalama kama kisingizio cha kuukwamisha mchakato huo wa kidemokrasia. Chama kikuu cha upinzani cha Nigeria, All Progressive Congress kimesema kuahirishwa kwa chaguzi hizo ni kikwazo kikubwa kwa demokrasia ya Nigeria na kimewataka Wanigeria wajiepushe na machafuko ili wasitumbukie katika mtego. Upinzani unaamini rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan anataka apate muda zaidi ili kuuondolea upinzani uungaji mkono, ambao umekuwa ukiimarika katika kura za maoni.